Tuesday, March 10, 2020

Afisa Nyuki wa TFS - Shamba la Miti Sao Hill Bw. Said Aboubakari akitoa elimu juu ya ufugaji nyuki na mazao yake katika uwanja wa bora jijini Dar Es Salaam ambapo mpambano wa mpira wa miguu ulikuwa ukiendelea.
Hadi mwisho wa mchezo wa leo timu ya KMC FC imeibuka kidedea baada ya kuifunga timu ya Sao Hill Forest SC goli 1 - 0
Mechi hizi za kirafiki zimeanza tangu tarehe 7/03/2020 ambapo timu ya Sao Hill Forest SC ilipangiwa kucheza na timu za Azam B, Simba B, X UDSM na KMC.
Ziara hii ya kimichezo ni matokeo ya michezo ya Misitu Sports Bonanza iliyokutanisha timu takribani 32 kutoka katika vijiji 60 vinavyolizunguka Shamba la Miti Sao Hill ambapo miongoni mwao walichaguliwa takribani wachezaji 20 ambao wameunda timu ya misitu iliyoko chini ya ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)- Shamba la miti saohill.
Aidha Lengo kuu la michezo hii ni kurudisha shukrani kwa jamii inayolizunguka shamba na kupitia michezo hii kunawasaidia vijana kujipatia ajira, kuvumbua vipaji vyao na kuviendeleza sanjari na kulitangaza shamba.
Tarehe 11/03/2020 timu ya Sao Hill Forest Forest SC itacheza na timu ya Simba B saa 08:00 Mchana katika Uwanja wa Uhuru.
Kauli Mbiu katika Michezo hii ni "UTUNZAJI WA RASILIMALI MISITU NA NYUKI NI JUKUMU LETU SOTE".

Pichani:Golikipa wa timu ya Taifa Tanzania Bw. Juma Kaseja akijipatia asali bora kutoka  TFS- Shamba la Miti Sao Hill.

Friday, March 6, 2020

Timu ya Mpira wa Miguu ya SaoHill Forest Sports Club kuwasili Dar es Salaam kwa Michezo ya kirafiki
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) - Shamba la Miti SaoHill kupitia timu yake ya mpira wa miguu leo tarehe 6/3/2020 inaelekea Dar es Salaam kutoka Mafinga, Wilayani Mufindi Mkoani Iringa kwa michezo ya kirafiki.
Kiongozi wa msafara huo na Mwenyakiti wa Misitu Sports Bonanza ambaye pia ni Afisa Nyuki wa Shamba la Miti SaoHill Bw. Said Aboubakari amesema timu itawasili Dar es Salaam leo na ipo tayari kwa michezo mbalimbali ya kirafiki ambayo itachezwa kwa siku tofauti ambapo itakutanisha SaoHill Forest Sports Club dhidi ya Azam B, KMC, Juhudi FC, na Simba B FC.
Ziara hii ya kimichezo ni matokeo ya michezo ya Misitu Sports Bonanza iliyokutanisha timu takribani 32 kutoka katika vijiji 60 vinavyolizunguka Shamba la Miti SaoHill ambapo miongoni mwao walichaguliwa takribani wachezaji 20 ambao wameunda timu ya Misitu iliyoko chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) - Shamba la Miti SaoHill.
Aidha lengo kuu la michezo hii ni nikurudisha shukrani kwa jamii inayolizunguka na shamba yaani(Corporate Social Responsibility) na kupitia michezo hii kunawasaidia vijana kujipatia ajira, kuvumbua vipaji vyao na kuviendeleza sanjari na kulitangaza Shamba.
Kauli mbiu katika michezo hii ni “UTUNZAJI WA RASLIMALI ZA MISITU NA NYUKI NI JUKUMU LETU SOTE”


Pichani: Timu ya Mpira wa miguu kutoka TFS - Shamba la Miti Sao Hill(Sao Hill Forest Sports Club).

Thursday, February 27, 2020

Shamba la Miti SaoHill kila mwaka hugawa miche kwa wananchi wa vijiji wanaolizunguka shamba ili waweze kupanda katika maeneo yao.
Zoezi hili hufanyika kila mwaka hasa katika msimu wa mvua ili kuhakikisha miti itakayopandwa ikue vizuri.
Hatua hii ya ugawaji wa miche ya miti husaidia kwa kiasi kikubwa kuwakumbusha wananchi juu ya uhifadhi wa misitu katika maeneo yao kwani wanapochukua miche hiyo huelekezwa namna na ya kuipanda na tunzaji wake.
Kwa mwaka 2019/2020 Shamba limegawa miche milioni moja kwa wananchi wanaolizunguka shamba ikiwa ni sehemu ya kusaidia na kuonyesha ushirikiano na jamii inayozunguka shamba.
Hata hivyo wananchi wameendelea kuhimizwa juu ya utunzaji wa miti wanayoipanda ili iwe na manufaa kwao na vizazi vijavyo.
Shamba la Miti SaoHill ni miongoni mwa mashamba 23 ya miti ya kupandwa ya serikali yanayosimamiwa na Wakala wa Huduma wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) lenye ukubwa wa hekta 135,903 ambazo zimehifadhiwa kwaajili ya upandaji miti kibiashara na hifadhi ya mazingira na vyanzo vya maji,makazi ya watumishi na uwekezaji.
Pichani: Wananchi wakiendelea kuchukua miche ya miti kutoka Tarafa ya Nne ya Shamba la Miti SaoHill - Mgololo.
#TUNZA MITI IKUTUNZE- MISITU NI MALI

Wednesday, February 19, 2020

Thursday, February 13, 2020


Wadau wa Mazao ya misitu waridhia uanzishwaji wa soko la pamoja

Wadau wa mazao ya misitu katika shamba la miti Saohill  wameridhia uanzishwaji wa soko la pamoja la mazao ya misitu katika Shamba la Miti SaoHill katika kikao kilichofanyika leo tarehe 13 Februari, 2020 katika ukumbi uliopo Shamba la Miti SaoHill.

Kaimu Meneja wa shamba Bw. Ignas Lupala  amewaeleza wadau kuwa serikali inaazimia kuanzishwa kwa soko la pamoja la mazao ya misitu ili kuwe na eneo moja ambalo wanunuzi watapata mbao bora na kwa urahisi .

Amesema kuwa uanzishwaji wa soko hili utasaidia wadau kuwa na uhakika wa kupata soko  na wanunuzi kuwa na eneo la uhakika la kupata bidhaa.

Naye Mwenyekiti wa wavunaji Shamba la Miti SaoHill Bw. Christian Ahia amesema kuwa suala la soko limekuwa ni chagamoto hivyo kwa uanzishwaji wa soko la pamoja utasaidia kuwaunganisha wavunaji.

Hata hivyo wadau wameipongeza serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kwa kuja na mpango wa uanzishaji wa soko la pamoja na  wameiomba serikali kuweka viwango vya mbao  kwani hivi sasa kumekuwa na mbao ambazo ni changa na hivyo kusababisa bei ya soko kuwa chini na hivyo kuwasababishia wao kupata hasara.

Kikao hiki kimeitishwa kufuatia maelekezo ya Naibu Kamisha Uhifadhi – Mipango na Masoko juu ya uanzishwaji wa soko la pamoja ili iwe rahisi katika upatikana wa masoko wa mazao ya misitu.

Pichani: Mwenyekiti wa Wavunaji shamba la Miti SaoHill Bw. Christian Ahia akizungumza wakati wa kikao cha kujadili juu ya uanzishwaji wa soko la pamoja la mzao ya misitu

Pichani: Kaimu Meneja wa Shamba la Miti SaoHill Bw. Ignas Lupala akizungumza na wadau wa mazao ya misitu wakati wa kikao cha kujadili juu ya uanzishwaji wa soko la pamoja la mazao ya misitu




Pichani Juu: Wadau wa mazao ya misitu katika Shamba la Miti SaoHill wakichangia mada wakati wa kikao cha kujadili juu ya uanzishwaji wa soko la pamoja la mazao ya misitu



Wednesday, February 5, 2020


WATUMISHI SHAMBA LA MITI SAOHILL WAPEWA ELIMU YA SHERIA
Watumishi wa TFS - Shamba la Miti SaoHill wamepatiwa mafunzo mbalimbali ya sheria ikiwa ni sehemuya maadhimisho ya siku ya sheria nchini yanayoendeshwa na Mahakama ya Tanzania. Lengo la mafunzo haya ni kutoa elimu kuhusu sheria mbalimbali ambazo wanazitumia katika shughuli za kazi za kila siku.
Mafunzo hayo yameendeshwa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Mahakama ya Tanzania, Uhamiaji, Maendeleo ya Jamii,Ardhi na Tume ya Usuluhishi na Migogoro ya kazi.
Katika mafunzo hayo watumishi wametakiwa kuwa waadilifu katika utendaji wao wa kazi, kufuata haki katika kuhudumia wananchi bila kubagua na pia kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa wakati.




Pichani: Meneja wa Shamba la Miti SaoHill Bw. Juma Mwita Msite akiongea wakati wa utoaji  wa elimu ya sheria iliyoratibiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania.

Pichani: Watumishi wa Shamba la Miti SaoHill wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa kuhusu sheria mbalimbali